MBUGA ZA WANYAMA MALEMA KILAMBO MBEYA.

Kwa muda mrefu tulikuwa tunasikia kama simulizi kwa wazee wetu kwamba miaka ya nyuma maeneo haya ya Malema (Kilambo) kulikuwa na mbuga iliyokuwa na wanyama wengi na wa aina mbali mbali kama ilivyo katika Mbuga zingine sasa, Ndipo Uyole cultural tourism enterprises (UCTE) kwa kushirikiana na Chai fm radio pamoja na Kingo super production (KSP) tukafunga safari ili kuweza kulichunguza hili kwa lengo la kupata uthibitisho kamili kutoka kwa Wenyeji na wazawa wa maeneo haya.

Tulifika katika kijiji cha Bwibuka kata ya Lupata wilaya ya Rungwe Halmashauri ya Busokelo mkoani Mbeya tuliweza kuoneshwa eneo ambalo yakadiliwa miaka 50 mpaka 60 iliyopita lilikuwa ni pori (Mbuga) kubwa na la kutisha sana ambalo wanyama walikuwa wakiishi humo, Eneo hili ndipo ilipo chemi chemi ya maji moto (Kilambo) na uoto wake ni wenye vichaka vichaka na miti mirefu michache, joto kiasi unao elekeana na ule upatikanao baadhi ya sehemu za Udzungwa katika safu za milima Livingstone.

Eneo hili lilianzia kilipo kibao cha shule ya Ntapisi mpaka maeneo jirani na Mbambo, Tulifanya mahojiano na Angetile Mwakalinga aliyezaliwa mwaka 1955 katika kijiji cha Bwibuka katika masimulizi yake alisema akiwa anakua aliweza kuona wanyama wadogo wadogo wa aina mbalimbali kwa maana wale wakubwa kwa asilimia kubwa walikuwa wameshaanza kutoweka.

Kwa mujibu wa Katabhila Mwakagile aliyezaliwa mwaka 1930 yeye katika masimulizi yake unagundua kwamba anaelezea uwepo wanyama wakubwa sana maana kipindi chake walikuwa bado hawatoweka wote, japo kadri miaka ilivyoendelea wanyama wakubwa wakaanza kutoweka, hivyo kwa mujibu wa masimulizi ya wote wawili tukapata kujua wanyama waliokuwepo ni pamoja na Imbawala (Mbawala), Amabhole (Chui) Amapatama (Fisi), Imbogo (Nyati), Ingulubhe sya ndisu (Nguruwe pori), Ingalamu (Simba), Sofu (Tembo), Kilungu (Nungu Nungu), Ngambili (Nyani) ambao wapo mpaka sasa.

Mara baada ya kupata maelezo haya tuliweza kuthibitisha hilo kwa kutumia vigezo mbalimbali tulivyovipata katika eneo husika ambavyo ni hali ya hewa na uoto wa eneo husika lililo karibu saana na safu za milima ya Livingstone ambayo hufanana kabisa na maeneo tofauti tofauti ikiwemo hifadhi ya Kitulo na Udzungwa, pia eneo lipo karibu saana na Hifadhi za mlima Rungwe na Kitulo ambapo baadhi ya wanyama walio tajwa hupatkana mpaka sasa kama vile Nyani aina kadhaa wa kadhaa, wanyama jamii ya Swala na jamii ya Chui ambao huonekana kwa uchache saana.

Vigezo vingine ni mahusiano na ukaribu wa eneo hilo na hifadhi za Kitulo, bonde la Usangu mpaka Hifadhi ya Ruaha Ambayo kwa njia mpya ya igawa inapatikana umbali wa KM 54 kutoka barabarani Igawa, ambapo inawezekana ndipo wanyama walikokimbilia na kuzuiwa na shughuli za binadam wasiweze kurejea tena.

Kwa sasa eneo hilo bado lina pori kidogo, na hakuna nyumba yoyote japo ukitokea Mbambo mpaka njia panda kilambo kuna nyumba zimejengwa ila si nyingi sana.


Comments