ZIWA NYASA (LAKE NYASA)

ZIWA Nyasa linaelezwa kuwa miongoni mwa maziwa makubwa yanayopatikana nchini Tanzania. Ziwa Nyasa haliko katika eneo la Tanzania pekee bali linagusa nchi tatu, zikiwemo Msumbiji na Malawi. Ramani mbalimbali za nchi ya Tanzania na pia za bara la Afrika zinaonesha mpaka kati ya Tanzania na Malawi upo katikati ya ziwa hilo kama ulivyo mpaka kati ya Msumbiji na Malawi.

Ofisa wa Mamlaka ya Maji ya Bonde la Ziwa Nyasa ambaye pia ni Mtaalamu Mkuu wa maji chini ya ardhi, Witgal Nkondola anasema kuwa ziwa hilo ni la tatu kwa ukubwa katika bara la Afrika; la kwanza likiwa ni ziwa Victoria linalofuatiwa na ziwa Tanganyika. Anasema ni bahati kwa Tanzania kumiliki sehemu ya maeneo ya maziwa hayo yote matatu yenye sifa ya ukubwa huo katika bara la Afrika.

“Ikumbukwe kuwa katika dunia, Ziwa Nyasa ni la nane kwa ukubwa duniani. Pia, katika Afrika ni ziwa la pili kwa kuwa na kina kirefu, ambapo lina kina chenye mita 705 likifuatiwa na Ziwa Tanganyika lenye kina cha mita 1500”, anasema.

Anasema, Ziwa Nyasa lina jumla ya Kilomita za mraba 29600, yaani urefu wa Kilomita 580 na upana wa kati ya kilomita 75 na 80. Anaeleza kuwa historia inaonesha kuwa Ziwa Nyasa ni matokeo ya Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki iliyotokea zaidi ya miaka 40,000 iliyopita.

“Ziwa hili lina maji baridi yasiyo ya chumvi kali kama ilivyo kwa maziwa mengine. Maji yake yana jotoridi la kati ya nyuzi joto 24 na 29,” anasema.

Hali hiyo ndiyo inayotajwa kuwa chanzo cha Ziwa Nyasa kuwa na zaidi ya aina 800 za samaki kuliko ziwa jingine lolote duniani. Anasema samaki wanaotumika kwa kitoweo pamoja na wa mapambo ni miongoni mwa wanaopatikana ndani ya ziwa hilo. Aidha, inaelezwa kuwa, uwepo wa fukwe nzuri na zisizo hatari kwa waogeleaji ni sifa nyingine ya Ziwa Nyasa.

“Ziwa hili halina samaki wakali wala mamba. Kwa upande wa Tanzania baadhi ya fukwe zilizopo pembezoni mwa ziwa hilo ni pamoja na Matema iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya, Mbamba Bay na Muhalo zilizopo wilayani Nyasa,”anasema.

Vivutio vingine vinatajwa kuwa ni bandari za Itungi au Kiwira za wilayani Kyela, Liuli na Mbamba Bay za wilayani Nyasa na Nsungu ya wilayani Ludewa.

Maji ya Ziwa Nyasa Mtaalamu huyo anasema kuwa maji ya Ziwa Nyasa yanatoka zaidi katika mito ya Tanzania na ndiyo inayoongoza kwa kumwaga maji mengi kwenye ziwa hilo. Anasema, mito hiyo huchangia zaidi ya asilimia 59 ya maji, ikifuatiwa na mito ya Malawi ambayo huchangia asilimia 33 na Msumbiji ikiwa ya mwisho kwa kuchangia asilimia nane pekee ya maji.

Anataja baadhi ya mito inayotiririsha maji katika ziwa Nyasa kuwa ni Songwe, Kiwira, Mbaka na Lufilyo iliyopo mkoani Mbeya. Kwa maelezo ya mtaalamu huyo, mto Lufilyo unajumuisha pia maji kutoka katika baadhi ya vijito vya wilayani Makete mkoani Njombe. Mito mingine kutoka Njombe ni Lumbila, Nkiwe, Mchuchuma na Luhuhu ambayo ndio inaingiza maji kwa kiasi kikubwa kuliko mito mingine yote.

“Mto Luhuhu una eneo la kidaka maji chenye ukubwa wa kilomita za mraba 13,000, wakati Songwe una eneo la kidaka maji chenye kilomita za mraba 4000. Mkoani Ruvuma ipo mito Lutukula, Mwinamaji, Mbawa, Lulekei na Chuwindi ambao ndio mpaka kati ya Tanzania na Msumbiji,” anaeleza.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Ziwa Nyasa ni la ajabu kidogo kwa sababu, licha ya kuwa na mito mingi inayoingiza maji ndani yake, lina mto mmoja pekee ambao hutoa maji hayo nje. Mto huo unatajwa kuwa ni mto Shire ambao unapita katika ardhi ya nchi ya Malawi ukitiririsha maji yake hadi mto Zambezi ambao nao hutiririsha maji yake bahari ya Hindi. Mto Shire huchangia kiasi cha asilimia 11.3 ya maji ya mto Zambezi.

Nkondola anasema, Watanzania wana kila sababu ya kujivunia nchi yao kuwa sehemu ya wamiliki wa ziwa hilo kutokana na kuwa wachangiaji wakubwa wa maji yaliyopo kwenye ziwa hilo, ikilinganishwa na Malawi na Msumbiji.

“Watanzania ndiyo wanaowezesha kwa kiasi kikubwa uwepo wa ziwa Nyasa. Kuchangia asilimia 59 ya maji si mchezo.Wasingetunza mito yao na vyanzo vingine vya maji kwa miaka hiyo yote leo hii yangekuwa yanazungumzwa mengine, ikiwemo kupungua kwa kina cha maji,” anasema.

Anaeleza kuwa mamlaka yao inapendekeza mipaka kati ya Tanzania na Malawi ibaki katikati ya ziwa kama sheria za mipaka za kimataifa zinazosema. Inaelezwa zaidi kuwa, hali ya uwepo wa mto mmoja pekee unaotoa maji kutoka ziwa Nyasa ni changamoto inayozifanya nchi za Tanzania na Msumbiji kutonufaika na maji yanayotoka ndani ya Ziwa Nyasa, licha ya kuwa zinachangia maji yanayoingia kwenye ziwa hilo. Malawi ndio inayofaidi maji yanayotoka ziwani humo, hivyo kuifanya Tanzania na Msumbiji kutofaidika sana, ingawa ndio nchi zenye mito inayomwaga maji mengi ziwa Nyasa.

Kwa mujibu wa Nkondola, Malawi inanufaika na maji ya Nyasa kupitia mto Shire uliobahatika kuwa na maporomoko na bonde lenye eneo tambarare.

Uwepo wa fursa Lifahamu Ziwa Nyasa na vivutio vyake kwa mataifa nMaji ya mito ya Tanzania ndio yanayolijaza zaidi Inaendelea hizo umekuwa chanzo cha nchi hiyo pekee inayoumiliki mto Shire kunufaika kwa uzalishaji umeme kupitia maporomoko ya Nkula yaliyopo katika mji wa Blanyre ambapo zaidi megawati 300 za umeme huzalishwa. Kilimo cha umwagiliaji cha mazao ya aina mbalimbali yakiwemo ya chakula hufanyika pia kwenye eneo la bonde tambarare.

Skimu za Lionde na Linthipe ni miongoni mwa miradi ya umwagiliaji inayotajwa kutumia maji ya mto Shire na ni miongoni mwa fursa kubwa za ajira kwa Wamalawi hususan vijana.

“Iwapo Tanzania ingekuwa na mto unaotoa maji ziwa Nyasa ingekuwa na fursa nyingi nzuri za ajira kwa vijana kama ilivyo Malawi katika mto Shire,” anasema.

Inaelezwa kuwa Tanzania haina shughuli kubwa za uzalishaji zinazowanufaisha wananchi wake kutokana na maji ya ziwa Nyasa, zaidi ya uvuvi duni na usafiri kwa njia ya maji. Anaongeza kuwa kutokana na hilo inaweza kuelezwa kuwa Watanzania hawajanufaika bado na maji wanayoyatunza na kuyaruhusu yaingie kwenye ziwa hilo. Hali hiyo inazua changamoto kwa Serikali kuhusu jambo linaloweza kufanywa kuhakikisha Watanzania wananufaika pia na maji hayo, kama ilivyo kwa wenzao wa Malawi.

“Upo umuhimu mkubwa kwa Serikali kushirikiana na wadau wengine kuanza mikakati ya uwekezaji wa nishati ya umeme kupitia vyanzo vya maji mbalimbali vilivyopo katika bonde la maji la Ziwa Nyasa”. “...Hii ni kutokana na mito pia iliyopo katika bonde hilo inayotiririsha maji yake ziwa Nyasa kutokuwa ya misimu. Hutiririsha maji mwaka mzima hivyo hakuna sekunde ambayo Tanzania haijawahi kuchangia maji yake ndani ya Nyasa,” anasema.

Ofisi ya Mamlaka ya Maji ya Bonde la Ziwa Nyasa inashauri Serikali kuona uwezekano wa kuwekeza katika uzalishaji wa nishati ya umeme ili isaidie kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nishati hiyo nchini. Anatoa mfano wa maporomoko ya mto Kiwira yenye uwezo wa kuzalisha megawati 24.6, mto Rumakari wenye maji pia ya kutoka mto Rumbila megawati 540, mto Luhuhu jumla ya megawati 602 na mto Songwe megawati 320, kwa bwawa la chini pekee.

Tayari vipo vyanzo 40 vinavyozalisha umeme kwa sasa ikiwa ni uwekezaji wa watu ama taasisi ndogo za binafsi. Ofisa huyo anapendekeza pia serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kutafuta uwezekano wa kuyatafutia matumizi maji yanayozalishwa nchini kabla ya kuingia katika ziwa Nyasa, ikiwemo shughuli za kilimo cha umwagiliaji, ujenzi wa mabwawa makubwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji samaki na matumizi ya kawaida ya maji majumbani pamoja na kuyahamisha welekeo kwenda katika maeneo yaliyo na uhaba wa maji.

“Tunashauri haya kutokana na watanzania kutonufaika na maji wanayoyatunza. Kupitia ziwa ni manufaa kidogo sana wanayapata. Kutokana na mitaji midogo wameshindwa kuyatumia pia maji katika mito yao kabla ya kuingia ziwani kwa shughuli za kilimo kwakuwa mito hiyo inapita kwenye maeneo yenye miteremko mkali. Hakuna tambarare ambayo ingewawezesha waendeshe kilimo cha umwagiliaji.”

“Ndio sababu tunashauri wadau kuwekeza katika umeme ama kutafuta uwezekano wa kubadili mwelekeo wa maji ya baadhi ya mito ili yaweze kusaidia katika shughuli nyingine za maendeleo, kwenye maeneo yanayokabiliwa na ukame,” anasema.

Ushauri wa mamlaka ya bonde la maji la ziwa Nyasa ni muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya Watanzania. Kwa muda mrefu maeneo mengi nchini. Kilimo ni miongoni mwa shughuli ambazo tumeshuhudia zikiwakomboa vijana kwa kuwapa ajira.

Lakini, miundombinu ya kuwawezesha kujikita kwenye ajira hiyo ndio changamoto kubwa inayosababisha wengi kutojiajiri katika shughuli hiyo.

Mifano ya maeneo yaliyotoa ajira kwa vijana katika kilimo ni Madibira, Mwendamtitu na Kapunga yaliyopo wilayani Mbarali mkoani Mbeya ambako kupitia kilimo cha mpunga cha umwagiliaji vijana wengi wameondokana na umasikini.

Si tu kwa kulima lakini hata kufanya shughuli katika mashamba ya wakulima wakubwa na kisha kulipwa ujira. Mpango wa kuzalisha umeme kupitia vyanzo vinavyotajwa na mamlaka ya bonde unaweza kuwainua watanzania wanaoishi maisha ya chini ya dola moja kwa kuwapa ajira mbalimbali walau za kuchaji betri za simu za watumiaji.

Chanzo: Habarileo

Comments